Msifuatishe Mwenendo wa Kizazi Hiki

Leo, majanga na matatizo mbalimbali yanaikumba dunia nzima: tishio la silaha za nyuklia za Korea Kaskazini, uchafuzi wa hewa na maji, uharibifu wa tabaka la ozoni na mifumo ya viumbe, mabadiliko ya hali ya hewa, matetemeko ya ardhi, njaa na ukame, ongezeko la watu, upotovu wa maadili, magonjwa mapya yasiyojulikana hapo awali na misiba mingine mingi.

Haya huitwa “ishara za mwisho wa dunia hii,” na yameandikwa katika Biblia yote. Katika Mathayo 24:3, mwanafunzi mmoja wa Yesu alimwuliza, “Tuambie, mambo hayo yatakuwa lini? Nayo ni nini dalili ya kuja kwako na ya mwisho wa dunia?” Yesu akajibu, “Taifa litaondoka kupigana na taifa, na ufalme kupigana na ufalme; kutakuwa na njaa na matetemeko ya nchi mahali mahali.”

“Kwa kuwa maasi yatazidi, upendo wa wengi utapoa. Tena habari njema ya ufalme itahubiriwa katika ulimwengu wote, kuwa ushuhuda kwa mataifa yote; hapo ndipo ule mwisho utakapokuja.” Sasa Injili ya Yesu Kristo inaenezwa duniani kote kupitia vyombo mbalimbali vya habari. Kama Danieli 12:4 inavyosema, “Wengi wataenda mbio huko na huko, na maarifa yataongezeka,” maendeleo ya usafiri wa leo huwawezesha watu kusafiri popote wanapotaka ndani ya siku moja.

Vivyo hivyo, maarifa yameongezeka. Maendeleo ya kisayansi ambayo wanadamu wamefanya katika miaka mia moja iliyopita ni makubwa kuliko yaliyofanywa katika miaka mia nne iliyotangulia. Maarifa mengi yameongezeka katika nyanja zote, zikiwemo jamii, utamaduni na uchumi. 2 Timotheo 3:1 na kuendelea inasema, “Lakini ufahamu neno hili, ya kuwa siku za mwisho kutakuwako nyakati za hatari.”

“Maana watu watakuwa wenye kujipenda wenyewe, wenye kupenda fedha, wenye kujisifu, wenye kiburi, wenye matukano, wasiotii wazazi wao, wasio na shukrani, wasio safi, wasiopenda watu wa kwao, wasiotaka kufanya suluhu, wasingiziaji, wasiojizuia, wakali, wasiopenda mema, wasaliti, wakaidi, wanaojivuna, wapendao anasa kuliko kumpenda Mungu.” Hizi ndizo tabia zinazoonekana katika jamii zetu leo. Watu wengi hujipenda wenyewe. Huvaa mapambo binafsi kama saa na vito vya thamani ghali, pamoja na mavazi ya kifahari kupita kiasi.

Nyakati nyingine hufuatilia mitindo kwa pupa sana, na kwa sababu ya fedha migogoro na matatizo hutokea kati ya wazazi na watoto, ndugu na wenzi wa ndoa. Wanaotazamwa kuwa viongozi wanapaswa kuweka mifano mizuri katika jamii zao, lakini hawasiti kutenda uhalifu kwa ajili ya faida zao wenyewe. Dhambi na uovu vimeenea kila mahali. Nyakati za maumivu na mateso za siku za mwisho zimefika.

Upendo wa watu wengi unapoa. Watu huwatelekeza watoto wao. Watoto huwapiga, huwasingizia na hata kuwaua wazazi wao. Uovu huu wa kukosa maadili umeenea katika jamii zote. (Hizi ni “ishara za mwisho wa dunia hii.”) Ninaomba kila mmoja wenu asifuate mwenendo wa dunia, bali aushinde kwa imani. Ninaomba haya katika jina la Bwana wetu!

    His Emeritus Bishop Dr. Jaerock Lee

Word of Life